Watu wawili wadungwa visu na washukiwa wa genge la uhalifu.


Watu wawili wanauguza majeraha baada ya kudungwa kwa visu na washukiwa wa genge la wahalifu katika mtaa wa Mshomoroni kule Kisauni Mombasa jioni ya jana.

Afisa mkuu wa polisi Kisauni Julius Kiragu anasema kwamba washukiwa hao wanakisiwa kuwa miongoni mwa wale walioachiliwa hivi majuzi kutoka korokoroni kupitia mpango wa kupunguza msongamano gerezani.

Kiragu anasema genge hilo ambalo idadi yake haijabaini lilianza kuwapora wapita njia muda mchache kabla ya saa moja jioni katika mtaa wa mshomoroni ambapo wawili hao walidungwa kwa kisu na kuporwa simu na pesa.

Hata hivyo kiragu anasema kwamba maafisa wa polisi waliokua wakishika doria waliwafyatulia risasi washukiwa hao ambao walitoroka huku mmoja wao akihofiwa kuroka na majeraha ya risasi.

Polisi wangali wanafanya msako wa washukiwa hao wanaoaminika kuwa genge la wahuni lililokuwa linatatiza wakaazi hapo awali.