Washukiwa wa pembe za ndovu kizimbani


Wanaume wawili wamefikishwa katika mahakama ya Narok na kushtakiwa kwa kosa la kupatikana na pembe 3 za ndovu zenye uzani wa kilo 30 na dhamani ya shilingi milioni 3 bila idhini kutoka kwa shirika la KWS.

Wanaume hao Simon Kipng’eno na Laban Sibilai wakishirikiana na wengine ambao hawakuwa mbele ya mahakama walipatikana na pembe hizo tarehe 5 mwezi huu wa Januari katika eneo la Oloolaimutia ¬†kaunti ndogo ya Narok magharibi.

Wakiwa mbele ya hakimu mkuu wa mahakama hiyo George Wakahiu wote wamekana mashtaka hayo.

Hakimu mkuu Wakahiu ameagiza kesi hiyo kusikizwa tarehe 11 Januari mwaka huu ambapo mahakama itatoa mwelekeo ikiwa wawili hao wataachiliwa kwa dhamana au la.

Hata hivyo, upande wa mashtaka umeomba mahakama hiyo isiwaachilie wawili hao huku ukidai kwamba itakuwa vigumu kuwakamata waliotoroka wawili hao watakapoachiliwa.