Wanahabari waliokuwa wamekwama Kapedo wanusuriwa


Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC inasema mfanyikazi wake mmoja alikuwa kati ya waliouawa katika eneo la Arabal Tiaty kaunti ya Baringo.

Katika taarifa, mwenyekiti wa tume hiyo wafula Chebukati amesema kuwa afisa msaidizi wa utawala katika tume hiyo eneo bunge la Tiaty Brian Silale alichukuliwa na watu wasiojulikana wakiwemo watu wengine 5 katika kituo cha kibiashara cha Chemolingot Tiaty saa tisa za mchana wa siku ya Jumanne lakinimwili wake ukapatikana hapo jana.

Chebukati amevitaka vyombo vya usalama nchini kuharakisha uchunguzi kuhusu mauaji hayo ya kinyama ili washukiwa wakabiliwe kisheria.

Hayo yanajiri huku wanahabari watatu waliokuwa wamekwama katika eneo la Kapedo kufuatia utovu wa usalama kunusuriwa.

Wanahabari hao wanaojumuisha Emmanuel Cheboit wa Radio Citizen, Peter Warutumo wa NTVna Mike Ekutan wa Radio Maisha wanasema wamekuwa wakijifungua ndani ya nyumba moja eneo la Kapedo kwa siku 7 baada ya hali kuwa mbaya.

Walilazimika kujificha baada ya wahalifu kumuua afisa wa ngazi ya juu wa kikosi cha GSU punde tu baada ya kukamilika kwa mkutano wa amani eneo hilo katika barabara waliyofaa kutumia.

Wamesema haya katika eneo la Kabarnet kaunti ya Baringo baada ya kuokolewa na maafisa wa polisi.