Wanafunzi wa shule ya msingi wafunga ndoa Migori


Polisi eneo la Kuria magharibi kaunti ya Migori kwa ushirikiano na idara ya watoto wanawasaka wazazi wanaodaiwa kuidhinisha harusi kati ya mvulana wa umri wa miaka 17 na msichana wa miaka 16.

Afisa mkuu wa idara ya watoto kaunti ndogo ya Kuria magharibi James Omondi anasema kuwa watoto hao wawili walitiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani hapo jana.

Omondi anasema wakiwa mahakamani walikiri kuwa ndoa yao ilikuwa imeidhinishwa na wazazi wao, wazazi wa mvulana wakitoa ng’ombe kama mahari.

Anasema kuwa wawili hao wamekuwa wakiishi kama mume na mke tangu mwezi Januari mwaka huu hadi walipokamatwa.

Mahakama ya Kehancha iliwaachilia huru na kuwekwa chini ya linzi wa shangazi na mjomba kesi hiyo ikitarajiwa kutajwa tarehe 23 mwezi ujao.