Wakaazi walalamikia kufungwa kwa mradi Kikambala.


SIku chache tu baada ya Mamlaka ya mazingira nchini NEMA kusitisha mradi wa shilingi bilioni mbili kule Kwakadzengo eneo la Kikambala kaunti ya Kilifi wakaazi wa eneo hilo sasa wamejitokeza na kumtaka Rais uhuru Kenyatta kuingilia kati ili kutatua mzozo unaozunguka utekelezaji wa mradi huo.

Bodi ya NEMA nchini chini ya wenyekiti wa John Konchela ilisitisha mradi huo kwa msingi kuwa ujenzi wake ulikiuka masharti ya Mazingira kama ilivyopendekezwa.

Wakaazi hao walipiga kambi katika lango kuu la Mradi huo wa Mzuri sweets Ltd wakidai kufunguliwa kwa mradi huo kwa misingi kuwa wameathirika kiuchumi baada ya kufungwa kwake.

Baadhi yao wanadai kuwa huenda wakapata hasara kubwa baada yao kuchukua mikopo kwa lengo la kufanya biashara na kampuni hiyo.

Haya yanajiri huku usimamizi wa kampuni hiyo kupitia maneja wa uzalishaji Mwalenga Magore ukizisuta vikali mamlaka husika kwa kile walichokitaja kama kukosa msimamo .