WAKAAZI WA KWALE WATAKIWA KUACHANA NA UVUMI KWAMBA ACHANI AMECHAGUA MGOMBEA MWENZA.


Wakaazi wa kaunti ya Kwale wametakiwa kupuuza habari zinazoenezwa mitandaoni kumhusu naibu gavana wa kaunti hiyo Fatuma Achani, kuwa tayari amemchagua mgombea mwenza wa kiti cha ugavana cha mwaka wa 2022.

Habari hizo zinadai kwamba ,Achani amemtangaza mwakilishi wa wadi ya Samburu Chengoni katika eneo bunge la Kinango ,Chirema Kombo, kama mgombea mwenza wa ugavana.

Hata hivyo, serikali ya kaunti ya Kwale imeandika kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba ,habari hizo zinalenga kumharibia jina naibu huyo wa gavana.

Mkurugenzi wa mawasiliano katika kaunti hiyo Daniel Nyassy ,ametaja habari hizo kuwa za uongo kwani ni propaganda zinazoenezwa na wapinzani wa Achani, hivyo kuwataka wakaazi kupuzilia mbali swala hilo.