Wafanyikazi wa KNH kuanza mgomo


Huduma za matibabu katika  hospitali ya kitaifa ya Kenyatta zinatarajiwa kuanza kutatizika kuanzia usiku wa mamane.

Hii ni baada ya mkutano kati ya vyama vya wahudumu wa afya katika hospitali hiyo na  tume ya kutathmini mishahara ya watumishi wa umma nchini SRC na wizara ya leba  kukosa kuzaa matunda mchana wa leo.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na chama cha madaktari nchini KMPDU , chama cha wauguzi nchini KNUN, wawakilishi wa KNH , chama cha wahudumu wasio wa afya Kenyatta KUDHEIHA, na SRC duru zinaarifu kuwa SRC imeshikilia kuwa inafaa kufanya ukaguzi upya kabla ya kuwapa nyongeza wanaohudumu katika hospitali hiyo ambayo ilipandishwa hadhi kutoka kiwango cha 3C hadi 7A.

Japo bunge liliidhinisha bajeti ya bodi ya KNH na wizara ya fedha kutoa fedha hizo mwaka 2012, maafikiano hayo hayajatekelezwa .

Aidha mgomo huo utadhiri pakubwa utoaji huduma hasa msimu huu wa janga la corona baada ya wahudumu wa afya kuwataka wananchi kutafuta huduma katika vituo vingine kuanzia kesho.