Wabunge kujadili janga la Covid-19 Jumatano ijayo


Bunge la kitaifa litaandaa kikao maalum Jumatano wiki ijayo kujadili maswala yanayohusiana na vita dhidi ya virusi vya Corona.

Kikao hicho kwa mujibu wa karani wa bunge la kitaifa Michael Sialai, kitakuwa cha kujadili hatua ambazo rais Uhuru Kenyatta ametangaza kwa nia ya kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Kulingana na mawasiliano kutoka kwa Sialai, spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi, ameridhia ombi la kiongozi wa wengi Aden Duale kwamba kikao maalum juma lijalo kiandaliwe kujadili janga hilo.

Kikao hicho kitaandaliwa kuanzia saa nne asubuhi kuangazia hazina iliyoundwa kufadhili vita dhidi ya Corona, bajeti ya ziada ambayo itasaidia kupiga jeki vita dhidi ya virusi hivyo miongoni mwa maswala mengine.