VIONGOZI WA PWANI WAKASHIFU MATAMSHI YA KARIGITHU, KUSEMA VIJANA PWANI HAWAJUI KIINGEREZA.


Viongozi kutoka Pwani wamemshtumu katibu mkuu wa maswala ya baharini Nancy Karigithu kuhusiana na matamshi yake kuhusu vijana wa Pwani kuwa chanzo cha kukosa nafasi za ajira kwenye sekta ya ubaharia ,ni kutokana na kutokuwa na ufasaha wa uzungumzaji wa lugha ya Kiingereza.

Akiongea mjini Mombasa mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ametaja matamshi hayo ,kama ya kuhuzunisha na yaliyolenga kuwadhalilisha vijana wa Pwani.

Mbunge huyo amesema kuwa chanzo cha vijana kukosa ajira katika sekta ya ubaharia sio ufasaha wa lugha ya kiingereza ,bali idara hiyo imekosa kuzifanyia kazi Sheria zilizopo ili kuwafaidi vijana.

Akiongeza kuwa atawasilisha hoja bungeni kumtaka katibu huyo kufika mbele ya bunge, kueleza kuhusu swala hilo.

Wakati huo huo amesema kuwa kama viongozi wa Pwani ,wataungana pamoja kukosoa viongozi wenye mawazo duni yanayonuia kuwavunja moyo vijana wa Pwani, ambao wanajizatiti katika sekta hiyo.

Katibu huyo alinukuliwa na gazeti moja humu nchini akisema kuwa, chanzo cha vijana wa Pwani kutoajiriwa katika sekta ya utalii ni ukosefu wa ufasaha katika lugha ya kiingereza.