Uchunguzi wa Ngumbao Jola falimia yadai haki


Hatimaye Familia ya mwendazake Ngumbao Jola aliyeuawa kwa kupigwa risasi mwaka jana wakati wa uchaguzi mdogo wa wadi ya Ganda huko Malindi kaunti ya Kilifi, sasa inalilia haki kuhusu mauwaji ya mpendwa wao.

Familia hiyo sasa inadai kuwa ni miezi mingi sasa tangu kifo cha mpendwa wao kujiri na kwamba serikali imesalia kimya kuhusu swala hilo.

Kulingana na mama mzazi wa Ngumbao Jola kwa kuuwawa kwa mwanawe kumeathiri pakubwa hali yao ya Maisha hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa aliyetegemewa katika familia hiyo.

Hamisi Mwangaya Yaa ambaye ni mmoja wa  familia hiyo ameyataka mashirika ya kijamii ya kutetea haki za kibinadamu kuingilia kati swala hilo ili ukweli ubainike na haki kupatikana.

Naye mwakilishi wadi ya  Ganda Reuben Katana, amesema tayari familia hiyo imemwandikia barua mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Nordin Hajj kutaka kujua matokea kuhusu uchunguzi wa kifo hicho.

Katana na wenzake wamesisitiza kwamba sharti wahusika wa mauaji hayo wakamatwe na kuchukuliwe hatua kali za kisheria.

Jola aliuawa kwa kupigwa risasi siku mbili kabla ya uchaguzi mdogo wa wadi ya Ganda mwezi Oktoba mwaka jana na hadi sasa swala hilo limesalia kitendawili.