Serikali yazuia mikutano ya kimataifa


Baada ya virusi vya Corona kutangazwa na shirika la afya ulimwenguni WHO kuwa janga la kimataiafa, serikali ya Kenya imeweka mikakati zaidi kuvidhibiti.

Baada ya kukutana na rais Uhuru Kenyatta kumjuza mikakati iliyowekwa, kamati ya dharura iliyobuniwa kuangazia jinsi taifa limejiandaa kudhibiti virusi hivyo, imetangaza kwamba wakenya wote sawa na wageni wengine wanaowasili nchini kutoka mataifa ambayo yameshuhudia virusi hivyo wajitenge kwa siku 14.

Kadhalika agizo la kuwazuia maafisa wa serikali kutoenda safari zisizo na umuhimu nje ya nchi litaanza kutekelezwa.

Aidha taasisi za elimu zimetakiwa kuzingatia usafi hasa kuosha mikono kwa kutumia sabuni, kando na machifu, viongozi wa kidini na wazee wa nyumba kumi kutakiwa kutoa hamasa kwa umma kuhusu virusi hivyo.

Huku haya yakijiri, huenda sasa kampuni za bima hazitagharamia matibabu ya virusi hivyo iwapo vitaingia nchini.

Masharti ya kampuni nyingi za bima huzizuia kulipia matibabu yanayotokana na vita au janga la kimataifa.