Safari ya BBI kukamilika leo


Muda wa kuhudumu wa Kamati ya kutathmini mustakabali wa taifa pamoja na mapendekezo ya kurekebisha katiba iliyobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga unatarajiwa kukamilika hii leo.

Kamati hiyo ya wanachama 14 inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa rais Kenyatta kuu ikiwa ushauri kuhusu mipango ya utekelezaji wa mapendekezo ya BBI.

Kamati hiyo iliyo chini ya mwenyekiti seneta wa Garissa Yusuf Haji itaangazia mbinu za kutekeleza mabadiliko hayo ya kisera na hata uongozi kwa mujibu wa kauli walizopokea katika vikao vyao.

Kando na viongiozi, taasisi na wanasiasa waliowasilisha maoni yao kwa kamati hiyo iliyoongezwa muda mwezi Januari mwaka huu, vilevile walipata fursa ya kupokea maoni kutoka kwa wananchi kupitia mikutano kadha iliyofanywa katika maeneo kadha nchini.

Hata hivyo, mikutano hiyo iliyokuwa imeanza kuibua joto la kisiasa nchini ilikamilika ghafla kufuatia janga la Covid-19 mapema mwezi Machi mwaka huu.

Bunge linapigiwa upatu kukumbatia mapendekezo ya kamati hiyo ikilinganishwa na kura ya maamuzi.