Rais Uhuru atoa changamoto kwa KDF


Rais Uhuru Kenyatta ameshauri Jeshi la Ulinzi nchini (KDF) kuekeza zaidi katika mafunzo ili kujiandaa vyema kukabili vitisho vya usalama vinavyoibuka.

Rais Kenyatta, amekariri kwamba mafunzo ni sharti yaangazie kutoa ujuzi utakaoandaa jeshi kukabiliana na changamoto mbali mbali kutoka nyanja za kawaida na zisizo za kawaida.

Rais amesema hayo katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Lanet, Kaunti ya Nakuru, ambako alizindua kundi la nane la maafisa wa Kadet ambalo limepata mafunzo ya miaka mitatu ya Shahada ya Sayansi ya Kijeshi na Usalama.

Maafisa hao wa Kadet, ambao walianza masomo hayo ya shahada inayotolewa na Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa ushirikiano na Wizara ya Ulinzi  mwaka wa 2017, watapewa vyeti vya kuhitimu mwezi ujao.

Akihutubia maafisa hao wanaofuzu, Rais Kenyatta amesema wanafaa kutumia ujuzi, utaalamu na uwezo waliopata  kuhudumia na kulinda uhuru wa taifa, raia wake na kanda.