Rais Kenyatta afungua upya uga wa Nyayo


KENYATTA NYAYO

Rais Uhuru Kenyatta amefungua tena uwanja wa michezo wa Nyayo  jijini Nairobi.

Rais amefungua uwanja huo wa Nyayo miaka mitatu baada ya kufungwa ili kufanyiwa ukarabati uliogharibu zaidi ya shilingi milioni 650.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi, rais Kenyatta ameshabikia ukarabati wa uga huo akitaja hatua hiyo kama mwanzo mpya katika michezo nchini.

Ameahidi ukarabati zaidi katika nyanja zaidi maeneo ya Eldoret Uasin Gishu, Marsabit, Nyeri, Kirigiti  Kiambu,  Wote  Makueni miongoni mwa nyanja zingine.

Uga wa nyayo ni miongoni mwa viwanja ambavyo vilikuwa vimepangiwa kutumika kuandaa michezo ya kuwania ubingwa wa bara africa mwezi januari mwaka 2018, lakini hilo likakosa kufanya baada ya kenya kupokonywa haki za kuandaa michezo hiyo kutokana na kwamba haikuwa tayari na miundo msingi hitajika.

Wakati huo huo, rais wa chama cha riadha nchini Paul Mutwii amesema kufunguliwa upya kwa uga wa Nyayo  kunajiri wakati mwafaka kwa jiji la Nairobi, ikizingatiwa Nairobi itakuwa mwenyeji wa mashindano ya riadha ya mabara yaliopewa jina ‘Kip Keino Classic’ ambayo yataandaliwa oktoba tarehe 3 katika uwanja huo ambao una nafasi ya watu 30,000.