MIPANGILIO YA ARDHI KWA WAKAAZI KUPATA HATI MILIKI -TANA RIVER.


 

Idara ya ardhi kaunti ya Tana River yatangaza mipango ya kuanza kutengeza ramani rasmi za mipangilio ya ardhi katika sehemu mbalimbali za makaazi, hatua ambayo itachangia wakaazi kupewa umiliki rasmi wa ardhi zao.

Miongoni mwa sehemu ambazo michoro hiyo ya ardhi inanuiwa kufanywa ni katika sehemu za Kone, Mikinduni, Bangale, Garsen, Madogo, kulingana na ilani ambayo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Mwanajuma Hiribae, huku moja wapo ya malengo ya mpango huo ikiwa ni kubainisha rasmi mipaka ya sehemu hizo za makaazi.

Wakazi wa sehemu hizo na washikadau mbalimbali wametakiwa kutoa maoni yao kuhusiana na mipango hiyo ya ardhi wakati ambapo kaunti inajiandaa kufungua rasmi sajili ya kwanza ya ardhi eneo hilo, baada ya kupata maabara ya kisasa .

Sajili hiyo inaanzishwa kwa ushirikiano na shirika la FAO ,hivyo itasaidia utengezaji hati miliki na stakabadhi zote za ardhi ,kwani wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakitumia sajili ya ardhi ya Lamu, Kilifi, Mombasa au hata Nairobi.