Mimba za mapema zapungua Kilifi wadai viongozi


Imebainika kuwa visa vya mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi katika kaunti ya Kilifi vimepungua kwa asilimia kubwa hivi sasa.

 

Kulingana na mbunge wa eneo la Kaloleni Paul Katana juhudi hizo zimeafikiwa kutokana na ushirikiano baina ya viongozi, wazazi, walimu na hata wanafunzi.

Mbunge huyo amesisitiza haja ya wakazi wa kaunti hiyo kuzingatia elimu kwa watoto wao kama njia moja wapo ya kukabiliana na changamoto ya umasikini.

Akizungumza huko Fumbini mjini Kilifi Katana amewataka wazazi kuacha kuingiza siasa katika masuala ya elimu na badala yake kujukumika kikamilifu katika maswala ya elimu kwa Watoto wao.

Amewashauri wazazi kutumia vyema fursa ya hazina ya ufadhili wa masomo inayotolewa na serikali ili kuhakikisha Watoto wao wanapata masomo.

Hayo yanajiri huku kamishina wa kaunti hiyo Magu Mutindika akisisitiza kuwa marufuku ya disco matanga ndiyo inayochangia pakubwa katika kupungua kwa visa  vya mimba za mapema kaunti hiyo.