Maelfu wahudhuria siku ya utalii Mombasa


Kwa mara ya kwanza wafanyibiashara katika sekta ya utalii Mombasa wameonyesha kuridhishwa na idadi ya wateja waliojitokeza kuhudhuria maadhimisho ya siku ya utalii katika bustani ya Mama Ngina Mjini Mombasa.

Katika  hafla hio iliyohudhuriwa na maelfu ya wananchi, wafanyibiashara wa Vinyago,  Nguo, wachoraji Hinnah na wauzaji wa vyakula  vya kitamaduni wamesema imekuwa afueni kwao kwa mara ya kwanza kibiashara tangu kuibuka kwa janga la Corona.

Katika ujumbe wao washikadau wa sekta hio wametoa wito kwa rais Uhuru Kenyatta kuondoa masharti yaliyowekwa kudhibiti janga la Corona wakitaka waruhusiwe kuendelea na biashara zao bila vikwazo.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla hio ni Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Wabunge Mishi Mboko wa Likoni Badi Twali wa Jomvu Senata wa Mombasa Mohamed Faki na Mwakilishi wa akinamama Bi Asha Hussein miongoni mwa wengine.

Hali ya usalama iliimarishwa katika uwanja huo uliojaa pomoni huku juhudi za kupima joto Kila aliyekuwa akifika uwanjani humo zikiambulia patupu kufuatia idadi kubwa ya watu.

Miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla hio kikosi cha waendeshaji baiskeli Kutoka Nairobi hadi kwenye hafla hio Mombasa.

Na katika kaunti ya Baringo washikadau kwenye sekta ya utalii hawakuwa na la kujivunia baada ya hoteli saba za kitalii katika eneo hilo kufurika maji baada ya Ziwa Baringo kujaa hadi kufurika.

Ni Hali wanayosema imechangia kaunti hio kupoteza takriban shilingi milioni 100 Kila mwezi kufuatia kupungua kwa watalii.