Macho yote kwa senate ugavi wa mapato ukiwa shabaha


Maseneta wanajiandaa kupiga kura kuhusu mgao wa pesa za kaunti alasiri ya leo kuhusiana na mswada wa ugavi wa rasilmali za umma.

Kiranja wa wengi katika bunge la senate Irungu Kang’ata ameambia radio Citizen kuwa tayari wameafikiana kuhusu mfumo maalum utakaotumiwa katika ugavi wa pesa hizo kila kaunti ikinufaika.

Kumekuwepo na tofauti kubwa kutoka kwa maseneta kuhusu mfumo bora, mikao minne ikikosa kuafikia lolote.

Mrengo wa Jubilee ulioshirikisha maseneta wanaoegemea mrengo wa naibu rais William Ruto hapo jana ulifanya mkutano wa faragha na kuafikiana kupitisha mswada huo chini ya uongozi wa kiranja wa wengi.

Hata hivyo, Naibu kiongozi wa wachache katika bunge hilo Cleophas malala anasema NASA haiungi mkono mswada huo.

Iwapo mswada huo utapitishwa basi kaunti 18 zitaathirika kwa kupokonywa kati ya shilingi milioni 300 na shilingi bilioni 1.8

Kaunti hizo ni pamoja na Wajir, Mandera Mombasa, Kilifi na Tharaka Nithi.

Nazo kaunti kama Vile Nandi, Uasin Gishu, Nakuru, Kirinyaga, Kiambu na kaunti zingine 22 zitapata nyongeza ya hadi shilingi bilioni 1.4.