JUMWA NA MWENZAKE KUJUA HATMA YAO KESHO KUHUSU KUACHILIWA KWA DHAMANA.


Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake Geoffrey Otieno watasalia tena kizuizini hii leo baada ya mahakama kukosa kutoa uamuzi kuhusu dhamana.

Mahakama kuu ya Mombasa inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu iwapo wawili hao ,wataachiliwa kwa dhamana au la hapo kesho.

Hii ni baada ya wawili hao kukana shtaka la mauwaji dhidi yao, mbele ya jaji Njoki Mwangi.

Mahakama ilielezwa kuwa mnamo tarehe 15 mwezi Oktoba mwaka 2019 katika wadi ya Ganda kaunti ya Kilifi, walimuua Ngumbao Jilo wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa wadi hiyo.

Upande wa mashtaka hata hivyo ulipinga kuachiliwa kwa dhamana kwa wawili hao ,wakidai kuwa watatatiza mashahidi na ushahidi uliopo.

Hata hivyo mawakili wao wakiongozwa na Jared Magolo, Douglas Omari na Cliff Ombeta wamepinga ombi hilo ,na kuitaka mahakama iwaachilie kwa dhamana kwani wamekuwa wakifuata maagizo ya mahakama.