Jiandaeni kwa amri ya kutotoka nje- Oguna


Serikali imewataka wakenya kuwa tayari kwa utekelezaji wa marufuku ya kutotoka nje inayotarajiwa kuanza kukumbatiwa kesho Ijumaa.

Msemaji wa serikali Kanali mstaafu Cyrus Oguna anasema kuwa kila mmoja anafaa kuwa nyumbani kabla ya marufuku hiyo kuanza kutekelezwa rasmi saa moja za jioni.

Marufuku hiyo ya kutotoka nje kwa muda wa saa 10 kote nchini ni ya pili baada ya ile iliyotolewa tarehe mosi mwezi Agosti mwaka wa 1982 baada ya jaribio la mapinduzi ya serikali ya arais wa pili wa taifa hili marehemu Daniel Toroitich arap Moi, mapunduzi yaliyotibuka.

Oguna akizungumza na Radio Citizen amewataka wananchi kuzingatia nidhamu ya hali ya juu kuhusiana na marufuku hiyo ili kuzuia maafisa wa usalama kuingilia kati.

Licha ya hayo,atakayehitaji msaada wakati wa marufuku hiyo ya kutoka saa moja za jioni hadi saa 11 za asubuhi atasaidiwa.

Hata hivyo, kuna watu wachache wanaotoa huduma hitajika wanaoruhusiwa kuwa nje wakati huo.