Hasara ya ghasia watu 2 wakiaga dunia kaunti ya Narok


Mtu mmoja ameuwawa mchana wa leo kwa kupigwa risasi huku wengine 3 akiwemo afisa wa polisi wakiuguza majeraha katika eneo la Olposimoru katika mpaka wa kaunti za Narok na Nakuru kufuatia vita kati ya jamii mbili hasimu eneo hilo.

Hii inafikisha idadi ya watu waliofariki dunia eneo hilo 2 baada ya mwanaume mwingine wa umri wa miaka 30 kuuwawa kwa kufumwa mishale hapo jana eneo hilo alipokuwa akichunga mifugo ndani ya msitu wa Mau.

Aidha, Ng’ombe 5 kutoka moja waliibiwa na katika hatua iliyoonekana ya kulipiza kisasi Ng’ombe 25 ya jamii ya pili wakaibwa, hali iliyochochea vurugu hata zaidi kati ya jamii hizo.

Kamishna wa kaunti ya Narok Samuel Kimiti ambaye alizuru eneo hilo la Olposimoru hii leo kujaribu kutuliza hali amesema kwamba wanachunguza mauaji ya mtu huyo ambaye amefariki dunia kwa kupigwa risasi kufuatia madai kwamba huenda alipigwa risasi na maafisa wa polisi.

Kimiti amesema kwamba waliojeruhiwa wamepelekwa katika hospitali ya rufaa ya Narok huku wengine wakipelekwa katika hospitali ya Olenguruone kaunti jirani ya Nakuru.

Hata hivyo, amesema kwamba hali ya amani imeanza kurejea eneo hilo baada ya maafisa zaidi wa usalama kutumwa kuthibiti hali.

Vita hivyo vinajiri wiki moja tu baada ya tume ya uwiano na utangamano nchini NCIC kumaliza misururu ya mikutano ya amani katika kaunti hiyo.

Haya yanajiri huku Mbunge wa Narok kaskazini Moitalel Ole Kenta akimtaka Waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiangi kuwaondoa askari wote kutoka jamii hizo mbili.