Category Archives: radio citizen

Mbunge wa Kasipul aachiliwa huru


Mbunge wa Kasipul Charles Ongodo ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi 15,000.

Hii ni baada ya kukiri shtaka la ukiukaji wa masharti ya kuzuia Covid-19 mbele ya Hakimu mkaazi wa mahakama ya Oyugis Celesa okore.

Alitiwa mbaroni jioni ya jana akidaiwa kukiuka masharti hayo kwa kuandaa mkutano eneo la Sino Rachuonyo na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Oyugis.
Hakuna waziri aliye na Covid-19- Mucheru


Waziri wa teknolojia ya mawasiliano joe Mucheru amekanusha ripoti kuwa kuna mawaziri waliothibitishwa kuwa na ugonjwa wa Covid-19.

Mucheru katika mahojiano ya kipekee amesema kuwa mawaziri wote walihudhuria mkutano wa baraza la mawaziri hapo jana na hakuna aliyeonyesha dalili za virusi vya Corona.

Hata hivyo, mawaziri Amina Mohammed wa michezo aliye nje ya nchi sawa na waziri Raphael Tuju anayeugua hawakuwepo.

Kumekuwa na madai katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa mawaziri watatu wamethibitishwa kuwa na virusi vya Corona.
Mbunge wa Kasipul kufikishwa kizimbani


Mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were anatarajiwa kufikishwa mahakamani hii leo.

Hii ni baada ya kutiwa mbaroni jioni ya jana akidaiwa kukiuka masharti ya kuzuia Covid-19.

Ong’ondo aliyezuiliwa katika kituo cha polisi cha Oyugis anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa mkuu wa polisi eneo la Nyanza Noah Mwivanda.
Sakaja kufikishwa kizimbani


Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja anatarajiwa kufika mahakamani hii leo.

Hii ni baada ya kutiwa mbaroni wikendi iliyopita akidaiwa kukiuka masharti ya Covid-19 kwa kuwa katika eneo la burudani wakati wa kafiu.

Uamuzi wa kufikiswha mahakamani uliafikiwa jana baada ya kuhojiwa katika afisi za DCI Kilimani hapa Nairobi.

Aidha alijiuzulu kutoka kwa kamati maalum inayoangazia utekelezaji wa masharti ya Covid-19.
Matumaini kwa maseneta kuamua mgao wa pesa kwa kaunti


Maseneta wanatarajiwa kuamua leo kuhusiana na mgao wa pesa zainazotarajiwa kupokezwa kauti mbalimbali nchini.

Hii ni baada ya tofauti kubwa kuibuka kati ya maseneta kuhusiana na mfumo unaotarajiwa kutumiwa kugawa zaidi ya shilingi bilioni 316 kwa kaunti nchini.

Nyufa zimeibuka kati ya maseneta hasa kutoka kaunti zinazotarajiwa kupoteza mgao mkubwa wa pesa hizo wakishinikiza mfumo utakaoridisha kila mmoja.

Licha ya hayo, Spika wa bunge la senate Ken Lusaka ameahidi kwamba bunge hilo litakubaliana kuhusu utata uliopo kuhusu ugavi wa fedha hizo za kaunti.

Lusaka anasema kikao cha leo kitafikia uamuzi kuhusu utata huo huku magavana wakiendelea kulalamikia kucheleweshwa kwa fedha.
Uongozi wa Jubilee watikiswa


Usimamzi wa chama cha Jubilee unaendelea kutikiswa na tofauti miongoni mwa viongozi wake.

Hii ni baada ya katibu mkuu wa chama hicho Raphael Tuju kupuzilia mbali shinikizo za naibu wake mbunge wa Soy Caleb Kositany kuweka wazi makadirio ya pesa za chama.

Tuju katika barua kwa Kositany amemsuta kwa kumshinikiza atoe maelezo hayo akidai maswala yaliyoibuliwa yanaweza tu kushughlikiwa na mwekahazina wa chama Alfred Mutai.

Hata hivyo, anasema wangali wanasubiri ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kuhusu matumizi ya pesa mwaka uliopita wa kifedha.
Maeneo ya kuabudia kurejelewa rasmi leo


Maeneo ya kuabudia yanatarajiwa kufunguliwa rasmi hii leo chini ya masharti mapya ya kuthibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Ni hatua inayojiri huku baadhi ya viongozi wa makanisa wakilalamikia masharti hayo wanayodai utekelezaji wake utakuwa Kibarua kigumu.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa baraza maalum la kidini lililotwikwa jukumu la kujadili kuhusu kurejelewa kwa maeneo ya kuabudia askofu Anthony Muheria amesisitiza kuwa masharti waliyotoa kuhusu utaratibu utakaofuatwa yatasalia yalivyo.

Muheria amesema baadhi ya viongozi wa kidini hawakufurahia masharti haya lakini akasema ni bora wayazingatie kwani huenda kuyakiuka kukawa na athari mbaya.

Kauli yake imeungwa na Askofu wa kanisa la kiangilikana, katika eneo la Gusii, John Omangi anayesema kuwa ni vyema ibada zianze kwanza na idadi ndogo ya waumini huku makanisa yakiangazia hali itakavyokuwa

Matumizi ya sabuni maalum ya kuua viini, maski kanisani na vifaa vya kupimia viwango vya joto ni kati ya yanayohitajika.

Masharti mengine ni pamoja na ibada kuhudhuriwa na waumini wasiozidi umri wa miaka 58,kuzuiwa kwa watoto wa umri chini ya umri wa miaka 13, usafishaji wa kanisa kila wakati, kutokaribiana kwa washiriki,muda wa saa moja wa ibada sawa na waumini wasiozidi 100.
SGR kurejelea shughuli leo


Huduma za Treni kati ya Nairobi na Mombasa zinatarajiwa kurejelewa asubuhi hii chini ya masharti makali ya kuzuia Covid-19.

Treni hizo zinatarajiwa kubeba asilimia 50 ya abiria, hii ikiwa abiria 600 kwa safari moja kulingana na maagizo yaliyotolewa na waziri wa uchukuzi James macharia.

Treni ya kwanza ya reli ya kisasa inatarajiwa kuondoka Nairobi saa mbili za asubuhi hii na kuwasili Mombasa saa saba kasoro.

Behewa moja litatengwa kwa ajili ya kushughulikia walio na dalili za virusi vya corona.
Maseneta kutatua mvutano kuhusu ugavi wa pesa


Bunge la Senate litaandaa kikao maalum hii leo kutanzua mgogoro kuhusu mfumo bora wa ugavi wa pesa za kaunti.

Ni baada ya baadhi ya maseneta kupinga mswada wa mfumo mpya wa ugavi wa mgao kwa serikali za kaunti unaozingatia zaidi idadi ya watu katika kaunti na sio ukubwa wake.

Ni mvutano uliofanya seneti kukosa kupitisha mswada huo na hivyo kuchelewesha mgao wa shilingi bilioni 316.5 pesa za mwaka huu wa kifedha.
Mchimba migodi aaga dunia Taita


Mchimba madini amefariki dunia baada ya kufunikwa na mchanga katika mgodi mmoja eneo la Kasighau eneo bunge la Voi kaunti ya Taita Taveta.

Inaarifiwa jamaa huyo alifunikwa baada ya mgodi kuporomoka huku wengine wawili wakinusurika bila majeraha yoyote.

Mwili wa mwanamume huyo unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya rufaa ya Moi mjini Voi huku uchunguzi ukianzishwa.

Kisa kama hicho sio cha kwanza kwani mwaka jana mgodi mwingine uliporomoka na kuwauwa watu watatu katika eneo hilo la Kasighau.