Category Archives: radio citizen

Nzige watua Kirinyaga


Kaunti ya Kirinyaga ni ya hivi punde kuvamiwa na nzige waharibifu.

Wakaazi wa eneo bunge la Gichugu wameelezea wasiwasi wao kutokana na nzige hao wanaoarifiwa kutua eneo hilo saa kumi na moja za jioni.

Maeneo ya Kamwana,Kiandimu,Githure,Ngariama na Kathunguri ndiyo yaliyoathirika zaidi, mimea ikiwemo majani chai ikiwa shabaha.
Watu wanne waathiriwa na Kipindupindu Murang’a


Serikali ya kaunti ya Murang’a imethibitisha kuwepo kwa ugonjwa wa kipindupindu.

Katika taarifa, afisa mkuu wa afya kaunti hiyo Muthui Gitonga amesema kuwa tayari kuna visa vinne vya kipindupindu ambavyo vimethibitishwa.

Waathiriwa kutoka mitaa ya Kayole na Mjini wametengwa katika chumba maalum katika hospitali ya murang’a Level 5

Kutokana na hilo, serikali ya kaunti imepiga marufuku uchuuzi wa chakula mjini humo.
Wandani wa Ruto wakosoa mikutano ya BBI


Viongozi wanaomuunga mkono naibu rais William ruto wamekosoa mikutano ya BBI inayoendelea nchini wakidai inatumika kuibua nyufa miongoni mwa wananchi.

Wakizungumza katika kanisa la Full gospel Gatunduri kaunti ya Embu, viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Mbeere kaskazini Muriuki Njagagua, ndindi nyoro wa Kiharu na Rigathi Gachagua wa Mathira wamesema kuwa kamwe hawatakubali kugawanywa na wanasiasa.

Aidha wamesema hawako tayari kuunga mkono nafasi zaidi za uongozi kupitia viongozi wa kieneo.
BBI yatakiwa kuangazia usalama Garissa na Mandera


Uhaba wa walimu katika ukanda wa Kaskazini Mashariki mwa nchi na hasa Garisa umetawala vinywa vya viongozi wa eneo hilo katika mkutano wa BBI unaoendelea kaunti ya Garissa.

Wakiongozwa na gavana wa Mandera Ali Roba na mwenzake wa Garisa Ali Korane, wametaka serikali kuziba mwanya uliopo kwa sasa.

Viongozi hao wanasema litakuwa jambo tupu kama masaibu ya wanafunzi wa kaunti hizo watasalia bila elimu.

Kwa upande wake kinara wa ODM Raila Odinga amewahakikishia wakazi wa eneo hilo kwamba atafanya kikao na rais Uhuru Kenyatta kutatua tatizo la uhaba wa walimu eneo hilo.

Raila amesema maswala ya elimu hayatatiliwa mzaha akisema wiki ijayo suluhu itapatikana.

Kiongozi huyo mesema kuwa ripoti ya BBI itaangazia pakubwa suala la ukosefu wa usalama.
Rais Uhuru atarajiwa kuzuru Nakuru


Rais Uhuru Kenyatta atajiunga na Wakristo wengine katika misa ya kuzindua kampeni ya kitaifa ya msimu wa Kwaresma wa Kanisa Katoliki katika Madhabahu ya Subukia, Kaunti ya Nakuru.

Katika Kanisa Katoliki, Kwaresma ni kipindi cha siku 40 cha kufunga na kujinyima, kusali na kutubu kabla ya Pasaka.

Kulingana na desturi ya Kikristo, msimu wa Kwaresma huanza Jumatano ya Majivu na kumalizika Jumapili ya Matawi na ni maadhimisho ya kila mwaka ambayo huwatayarisha waumini, kupitia sala, toba, kutoa zaka na kujinyima, kwa matukio yanayohusiana na mateso ya Yesu msalabani, na maadhimisho ya kufufuka kwake.

Rais pia atashuhudia kuzinduliwa kwa Waraka wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki ambapo maaskofu hao huwahimiza Wakristo wote na wahisani kuungana na kukabiliana na matatizo yanayokumba jamii huku wakitetea mabadiliko nchini.
Hofu nzige wakitua Laikipia


Kaunti ya Laikipia ni ya hivi punde kuathiriwa na nzige wakaazi wakohofia uharibifu zaidi baada ya wadudu hao waharibifu kutua kaunti hiyo jioni ya jana.

Wakaazi tuliozungumza nao wanasema kuwa tayari nzige hao wameanza kuharibu mimea yao.

Salama, Kalampton, Lorian, Mihianyu, Ng’arua na Kiandege ni kati ya maeneo yaliyovamiwa na nzige hao.

Waziri wa kilimo kaunti hiyo James Mwongere amesema kuwa serikali kwa sasa inatupia jicho nzige hao ili kubaini dawa bora ya kuwazima.
Polisi korokoroni akidaiwa kumnajisi mwanafunzi


Afisa mmoja wa magereza anayehudumu katika kituo cha Tambach kaunti ndogo ya Keiyo kaskazini kaunti ya Elgeyo Marakwet anazuiliwa katika kituo hicho akidaiwa kumnajisi mwanafunzi wa shule ya upili ya Sing’ore.

Inadaiwa kuwa wakazi wa eneo hilo walivamia nyumba ya afisa huyo na kumpata akimtendea mwanafunzi huyo unyama huo.

Wazazi wa mwanfunzi huyo wanasema kuwa mwanao alitoweka hapo jana kabla yao kupata ripoti kutoka kwa wanachi kuwa mwanafunzi huyo alionekana kwa nyumba ya afisa huyo hii leo.

Hata hivyo wazazi hao wamelaani kitendo hicho huku wakitaka serikali kuhakikisha kuwa mwanao amepata haki na afisa huyo kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Raia wa pakistan waachiliwa huru Mombasa


Mahakama ya Mombasa imewaachilia kwa dhamana ya shillingi million 20 wafanyibiashara wawili raia wa Pakistan baada ya kukwepa kulipa ushuru wa shillingi billioni 1.5.

Wawili hao Rahim Qasim na Rameez Gulzar Ali, wamefikishwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Mombasa Edna Nyaloti na kukabiliwa na mashtaka matatu ya kukwepa kulipa ushuru.

Mahakama imeelezwa kuwa kati ya mwaka 2016 na 2019 wawili hao wakiwa wakurugenzi wa kampuni ya Jhulay Lal Commodities Limited walikwepa kulipa ushuru wa zaidi ya shillingi million 500 mwaka 2016.

Mashtaka mengine ni kuwa wafanyibiashara hao walikwepa kulipa ushuru wa zaidi ya million 400 mwaka 2017 na ushuru wa zaidi ya millioni 520 mwaka 2018.

Mahakama pia imewaamuru wasalimishe pasipoti zao za usafiri.

Kesi hiyo itatajwa tarehe 3 mwezi Machi mwaka huu.
Familia ya Sergeant Kenei yataka haki


Familia ya afisa wa polisi aliyekuwa akihudumu jumba la afisi ya naibu rais na aliyepatikana ameaga dunia hapo jana imeelezea haja ya uchunguzi wa kina kuhusiana na kifo cha mwanao.

Akihutubia wanahabari nyumbani kwake kijiji cha Chemasis,Rongai kaunti ya Nakuru, babake John Chesang amesema kuwa alishangaa kubaini kupitia vyombo vya habari kuwa mwanaye Kipyegon Kenei alikuwa ameaga dunia bila kupewa maelezo rasmi na serikali.

Naye nduguye Emmanuel Kenei amesema marehemu kamwe hakuwa na ishara za msongo wa kimawazo alipoenda kule kumtazama mwanaye wa siku 5.

Familia hiyo sasa inashinikiza uchunguzi utakaowapa haki wakisema wanaamini mwanao hakujiua inavyodaiwa.
Raia wa uchina wakamatwa wakitoroka


Maafisa wa DCI wamewatia mbaroni raia watatu wa kichina waliokuwa wakijaribu kutoroka nchini kupitia uwanja wa kimataifa wa ndege wa jomo Kenyatta.

Liao Boping, Lu Jianfang na Li Linrong ni kati ya watalii 5 kutoka uchina waliokamatwa na kushtakiwa katika mahakama ya nakuru tarehe 17 mwezi January kwa kuuza mashine za kamari zilizopigwa marufuku bila vibali.

Raia hao walikuwa wamepata paspoti zingine mpya baada ya kutakiwa kuzirejesha za hapo awali.