Category Archives: bahari fm

VIONGOZI WATETEA MADAI KUWA CHAMA CHA ODM KIMEPOTEZA UMAARUFU,KILIFI.


Baadhi ya viongozi wa mrengo wa ODM kutoka kaunti ya Kilifi hatimaye wamejitokeza na kupuzilia mbali tetesi kuwa chama cha ODM kimepoteza umaarufu eneo hilo.

Mwakilishi wa wadi ya Kakuyuni kaunti ya Kilifi Nickson Mramba, amesisitiza kuwa chama hicho kingali imara eneo hilo, na kwamba kauli hizo ni poroja zisizo msingi.

Katika taarifa yake kule mjini Malindi, Mramba amesema kuwa huenda wanaoeneza uvumi huo, wanatumiwa na wanasiasa nchini kukipaka matope chama hicho.

Hata hivyo Mramba amewaonya viongozi wa kisiasa dhidi ya kuwatumia wafuasi wao kuwatusi viongozi wengine ,katika mitandao ya kijamii.
ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 2.8 ZADAIWA KUPOTEA, KATIKA HARAKATI ZA UJENZI WA CHUO CHA UTALII VIPINGO.


Huku ujenzi wa chuo cha utalii kule vipingo ukisitishwa , Zaidi ya shilingi bilioni 2.8 zimedaiwa kupotea katika mazingira tata.

Kulingana na Mbunge wa Kilifi kaskazini Owen Baya amesema pesa hizo ,zimekuwa zikilipwa wadau mbali mbali wanaohusika na ujenzi huo kwa manufaa ya kibinafsi badala ya ujenzi huo.

Chuo hicho kilitarajiwa kukamilika tangu mwaka wa 2017, lakini idara husika haijatekeleza majukumu yake ipaswavyo ndiposa mradi huo umekwama.

Hata hivyo mbunge huyo ameahidi kusimama kidete katika kuhakikisha mradi huo unakamilika ,ili wananchi waweze kufaidika.

Amedai kucheleweshwa kwa mradi huo kumechangia pakubwa katika kudorora kwa sekta ya utalii nchini ,kutokana na uhaba wa wafanyikazi waliohitimu katika taaluma hiyo.
MTOTO WA SHULE AZAMA BAHARINI SHELLY BEACH,MOMBASA.


Mtoto anayekisiwa kuwa kati ya umri wa miaka 12 amefariki baada ya kuzama maji alipokuwa akiogelea katika eneo la Mkunazini Shelly Beach, Likoni kaunti ya Mombasa.

Kulingana na Ali Said ,ambaye ni msimamizi wa ufuo eneo hilo ,alipata ujumbe huo kutoka kwa kijana mmoja ambaye ameona mwili unaelea katika eneo hilo.

Said amesema kuwa huenda kijana huyo alikuwa na wenzake ambao walitoroka kwani walipata nguo zake ufuoni.

Tayari Mwili umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali kuu kanda ya Pwani,huku akitoa wito kwa wazazi kutowaruhusu watoto wao kuja baharini kuogelea, kwani ni hatari kwa usalama wao.
ZAIDI YA WAKAAZI ELFU 20 WAKOSA VITAMBULISHO TAITA TAVETA.


Zaidi ya watu 20,000 wakiwemo baadhi ya wakaazi wa kaunti ya Taita Taveta wanaitaka serikali kuwatambua kama wakenya kwa kuwapa vitambulisho. 
 
Wananchi hao ambao baadhi yao ni wafanyikazi waliyostaafu wanasema hawajapata malipo yao ya kustaafu huku wengine wakosa kuajiriwa sawa na kunyimwa huduma mbalimbali muhimu kimaisha, kisa na maana ni kukosa stakabadhi mhimu ya kitambulisho cha kitaifa. 
 
Kwa sasa wanasema huenda ikawa vigumu kushiriki katika kura ya mwaka 2022 iwapo watakosa stakabadhi hiyo muhimu.WAZIRI WA FEDHA TANA RIVER MBELE YA KAMATI YA BUNGE,KUJITETEA KWA MCHAKATO WA KUMNG’ATUA.


Waziri wa Fedha kaunti ya Tana River, Mathew Babwoya, atalazimika kufika mbele ya kamati spesheli ya bunge la kaunti kujitetea baada ya wawakilishi wadi kuanza mchakato wa kumng’oa afisini.

Bunge limeidhinisha hoja ya kumng’atua mamlakani waziri huyo ,ambayo imewasilishwa na Naibu Kiongozi wa wengi, Salim Bonaya, kwa madai ya matumizi mabaya ya mamlaka, kukiuka katiba na kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Kamati hiyo ya bunge ya watu watano itaongozwa na Ismail Kodobo, na inatarajiwa kumhoji waziri dhidi ya madai yaliyotolewa na kisha kuwasilisha ripoti kwa bunge kuidhinishwa au kuangushwa.
WANAWAKE WAWILI WATIWA NGUVUNI KWA MADAI YA KUWAKEKEA WATOTO 2 , TANA RIVER.


Wanawake wawili wenye umri wa miaka 48 na 81 wakamatwa na polisi kaunti ya Tana River kwa madai ya kukeketa wasichana wawili wadogo wa miaka mitano5 na mwengine miaka 7 katika kijiji cha Sombo .

Aidha, watoto hao wamelazwa katika hospitali kuu ya kaunti ya Garissa kwa matibabu zaidi ,huku wanawake hao wawili ambao inasemekana ndio waliowakeketa wakizuiliwa na polisi katika kituo cha polisi cha Madogo.

Kamanda wa polisi Tana River, Fredrick Ochieng anasema watafikishwa mahakamani hapo kesho na kujibu mashtaka kulingana na sheria dhidi ya ukeketaji.

Hata hivyo, vifaa vilivyotumika katika ukeketaji huo havikupatikana ,huku Ochieng akionya wakazi dhidi ya mila hiyo iliyopitwa na wakati.
WAKAAZI WA KWALE WATAKIWA KUACHANA NA UVUMI KWAMBA ACHANI AMECHAGUA MGOMBEA MWENZA.


Wakaazi wa kaunti ya Kwale wametakiwa kupuuza habari zinazoenezwa mitandaoni kumhusu naibu gavana wa kaunti hiyo Fatuma Achani, kuwa tayari amemchagua mgombea mwenza wa kiti cha ugavana cha mwaka wa 2022.

Habari hizo zinadai kwamba ,Achani amemtangaza mwakilishi wa wadi ya Samburu Chengoni katika eneo bunge la Kinango ,Chirema Kombo, kama mgombea mwenza wa ugavana.

Hata hivyo, serikali ya kaunti ya Kwale imeandika kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba ,habari hizo zinalenga kumharibia jina naibu huyo wa gavana.

Mkurugenzi wa mawasiliano katika kaunti hiyo Daniel Nyassy ,ametaja habari hizo kuwa za uongo kwani ni propaganda zinazoenezwa na wapinzani wa Achani, hivyo kuwataka wakaazi kupuzilia mbali swala hilo.
MAAFISA WA UTAWALA WAMULIKWA, TAITA TAVETA.


Mashirika mbali mbali ya kutetea haki za kibinadamu kaunti ya Taita Taveta yameshtumu baadhi ya maafisa wa utawala kaunti hiyo kwa kuchangia ongezeko la dhulma kwa mtoto wa kike.

Wamesema kuwa hatua ya polisi kuwaachia huru baadhi ya washukiwa wa dhulma hizo inawafisha moyo licha yao kuwa na ushahidi wa kutosha kuona wahusika wanafunguliwa mashtaka.

Aidha wamesema kuwa ongezeko la visa vya kina baba kuwadhuluma wanao wa kike wa kambo limeongezeka pakubwa kaunti hiyo huku akihusisha ongezeko la visa hivyo kuchangiwa na baadhi ya wakazi kukosa kupiga ripoti kwa idara zinazohusika.
HUDUMA ZA AFYA ZIKO DUNI.


Kiongozi wa jamii kaunti ya Lamu Phyllip Mbuthia amehuzunishwa kuona kila siku wakaazi wa Lamu wanalazimika kusafirishwa hospitali zizilioko nje ya kaunti ya Lamu ili kusaka huduma za matibabu.

Mbuthia amemtaka Gavana wa Lamu Fahim Twaha kujukumika ipasavyo  na kuboresha sekta ya afya Kaunti ya Lamu ili wakaazi wapate huduma za matibabu kwa ukaribu na haraka.

Kadhalka ametaka serikali ya kaunti ya Lamu kupitia Idara ya Afya kuboresha huduma za afya kwa kueka madawa ya kutosha sawa na vifaa hitajika mahospitalini.

Wakaazi wengi kaunti ya Lamu wamefariki njiani wanapokuwa wakisafirishwa hospitali za nje kusaka matibabu zaidi kutokana na ukosefu wa huduma nyingi Lamu.
KERO LA WANYAMA PORI, KWALE.


Wakaazi wa Barcelona katika kijiji cha Mwaweche huko Msambweni kaunti ya Kwale wanalalamikia kuhangaishwa na uvamizi wa wanyamapori katika eneo hilo.

 Wakiongozwa na Janet Olenyawa, wakaazi hao ambao ni wakulima eneo hilo wanasema kuwa mimea yao inavamiwa shambani na wanyama hasa tumbiri na nguruwe.

Sasa wakaazi hao wanaitaka serikali kupitia shirika la wanyamapori nchini KWS kuingilia kati kwa kuwa hali hiyo imeathiri pia masomo ya watoto shuleni.

Pia wamelalamikia kuhangaishwa na nyati wanaovamia mashamba ya wakaazi kando na nyoka wanaohatarisha pakubwa maisha yao.